Aliyewatumia wanafunzi kuchimba kaburi akamatwa.
Jeshi la Polisi Mkoani Rukwa, linamshikilia mtu mmoja Tanda Thadeo (30),mkazi wa kitongoji cha Kasisiwe kilichopo manispaa ya Sumbawanga kwa tuhuma za kuwatumia wanafunzi kushiriki zoezi la kufukua kaburi la mtoto ili afufuliwe.
Kamanda wa Polisi Mkoani humo, ACP Theopita Mallya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa Thadeo anashikiliwa kwa tuhuma za kuwatumia wanafunzi hao wa Darasa la sita katika Shule ya Msingi Kasisiwe iliyopo Manispaa ya Sumbawanga, kwa kuwaahidi ya malipo ya shilingi elfu kumi.
“Mtuhumiwa alifanya tukio hilo ikidaiwa kuwa wanataka kumfufua mwanae na watoto waliofanya kazi hii walipewa ahadi ya malipo ya shilingi elfu kumi,” amesema Kamanda Mallya.
Mtoto huyo Martine Tanda (2) anayedaiwa kutaka kufufuliwa alifariki na kuzikwa Juni 17, 2022 katika makaburi ya kitongoji cha Kasisiwe kilichopo Mkoani Rukwa
Aidha kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi wilaya ya Sumbawanga, Marry Kway naye alishiriki katika kutoa somo la ukatili wa kijinsia na namna ya kuripoti matukio ya kihalifu kwa wanafunzi wa shule hiyo, ili kupunguza vitendo vya uvunjifu wa amani katika jamii.
Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoani humo limekemea vitendo vya kihalifu na kusema kuwa halita mvumilia mtu yeyote atakayejihusisha na matukio ya uvunjifu wa sheria.
Imeandikwa na Rafael Masau
Comments